Luke 7

Isa Amponya Mtumishi Wa Jemadari

(Mathayo 8:5-13)

1 aBaada ya Isa kumaliza kusema haya yote watu wakiwa wanamsikiliza, akaingia Kapernaumu. 2 bMtumishi wa jemadari mmoja wa Kirumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu kufa. 3Jemadari huyo aliposikia habari za Isa, aliwatuma wazee wa Kiyahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari. 4Wale wazee walipofika kwa Isa, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili, 5kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.” 6Hivyo Isa akaongozana nao, lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Isa, “Bwana, usijisumbue, kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. 7 cNdiyo maana sikujiona hata ninastahili kuja kwako wewe. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. 8Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”

9Isa aliposikia maneno haya, alishangazwa naye sana. Akaugeukia ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.” 10Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Isa waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.

Isa Amfufua Mwana Wa Mjane

11Baadaye kidogo, Isa alikwenda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walikwenda pamoja naye. 12 dAlipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke. 13 eBwana Isa alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”

14 fKisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.” 15 gYule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Isa akamkabidhi kwa mama yake.

16 hWatu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu, Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” 17 iHabari hizi za mambo aliyoyafanya Isa zikaenea Uyahudi wote na sehemu zote za jirani.

Isa Na Yahya Mbatizaji

(Mathayo 11:2-19)

18 jWanafunzi wa Yahya Mbatizaji wakamweleza Yahya mambo haya yote. Hivyo Yahya akawaita wanafunzi wake wawili 19 kna kuwatuma kwa Bwana ili kumuuliza, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

20Wale watu walipofika kwa Isa wakamwambia, “Yahya Mbatizaji ametutuma tukuulize, ‘Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?’ ”

21 lWakati huo huo, Isa aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, na pia akawafungua vipofu wengi macho wakapata kuona. 22 mHivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yahya yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema. 23Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

24 nWajumbe wa Yahya walipoondoka, Isa akaanza kusema na makutano kuhusu Yahya Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipokwenda kule nyikani, mlikwenda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo? 25Kama sivyo, mlikwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha, watu wanaovaa mavazi ya kifahari na kuishi maisha ya anasa wako katika majumba ya kifalme. 26 oLakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii. 27 pHuyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa: “ ‘Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,
atakayetengeneza njia mbele yako.’

28 qNawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hakuna aliye mkuu kuliko Yahya. Lakini yeye aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yahya.”

29 r(Watu wote hata watoza ushuru waliposikia maneno ya Isa, walikubali kwamba mpango wa Mungu ni haki, maana walikuwa wamebatizwa na Yahya. 30 sLakini Mafarisayo na wataalamu wa sheria walikataa mpango wa Mungu kwao kwa kutokubali kubatizwa na Yahya.)

31Isa akawauliza, “Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Wanafanana na nini? 32Wao ni kama watoto waliokaa sokoni wakiitana wao kwa wao, wakisema: “ ‘Tuliwapigia filimbi,
lakini hamkucheza;
tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,
lakini hamkulia.’

33 tKwa maana Yahya Mbatizaji alikuja, alikuwa hali mkate wala hanywi divai, nanyi mkasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’ 34 uMwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ 35 vNayo hekima huthibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote.”

Isa Apakwa Mafuta Na Mwanamke Mwenye Dhambi

36 wBasi Farisayo mmoja alimwalika Isa nyumbani kwake kwa chakula. Hivyo Isa akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kukaa katika nafasi yake mezani. 37Naye mwanamke mmoja kwenye ule mji, ambaye alikuwa mwenye dhambi, alipojua kwamba Isa alikuwa akila chakula nyumbani kwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato. 38 xYule mwanamke akasimama nyuma ya miguu ya Isa akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake, akaibusu na kuimiminia manukato.

39 yYule Farisayo aliyemwalika Isa alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa, na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani, na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.”

40Isa akanena akamwambia, “Simoni, nina jambo la kukuambia.”

Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.”

41“Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari 500
Dinari 500 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku mia tano.
na mwingine dinari hamsini.
42Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda yule aliyewasamehe zaidi?”

43Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.”

Naye Isa akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.”

44 aaKisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake, na kunifuta kwa nywele zake. 45 abHukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia. 46 acHukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato. 47 adKwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”

48 aeKisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”

49 afLakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?”

50 agIsa akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”
Copyright information for SwhKC